Hakim Abulqasim Mansour Ferdowsi

Hakim Abulqasim Mansour Ferdowsi

Hakim Abulqasim Mansour Ferdowsi

Hakim Abulqasim Mansour Ferdowsi mtaalamu wa fasihi na malenga mkubwa wa Iran, alizaliwa mwaka 319 Hijiria Shamsia (Kalenda ya Kiirani) ambayo ni sawa na mwaka 935 Miladia katika mji wa Tous, ulioko kaskazini mashariki mwa Iran. Familia ya Ferdowsi ilikuwa ya wakulima, na baba yake alikuwa na ardhi kubwa ya kilimo na tajiri pia, na kwa sababu hii, Ferdowsi aliishi kwa faraja wakati wa ujana wake.

 

Kwa utajiri huo aliokuwa nao baba yake, ulimwezesha Ferdowsi kutumia ujana wake kusoma historia na kupata maarifa zaidi. Kadiri Ferdowsi alivyozidi kusoma historia ya Iran, ndivyo alivyopendezwa zaidi na hadithi na ngano za kale za Kiirani; kiasi kwamba aliamua kuandika mkusanyiko mkubwa wa hadithi za Kiirani. Nyakati za utoto za Ferdowsi ziliambatana na utawala wa nasaba ya Wasamanid, na wafalme wa Samanid walipendezwa sana na fasihi ya Iran.

Tarehe kamili ya ndoa ya Ferdowsi haijatajwa kwenye vyanzo vya historia, lakini malenga huyo alijaaliwa kuwapata watoto wawili, mmoja wa kiume ambaye alifariki dunia wakati wa uhai wa baba yake, pia mtoto wake mwengine alikuwa wa kike.

Malenga huyu alianza kusoma mashairi akiwa kijana mdogo ambapo hadi mwishoni mwa umri wake alijikita katika kuboresha fani yake hiyo. Miongoni mwa athari muhimu za malenga huyo wa Kiirani ni kitabu alichokipa jina la "Shahnameh Ferdowsi" kilichokuwa na beti elfu hamsini kiliandikwa katika karne ya tano. Kitabu hicho kilichosheheni historia ya jadi na utamaduni wa Iran kabla ya ujio wa Uislamu, kimefasiriwa katika lugha mbali mbali duniani. 

Utenzi huu umepewa hadhi ya kitaifa na kuwa utenzi wa taifa la Iran kutokana na maudhui yake. Shahname "Kitabu cha Wafalme" ni utenzi unaoelezea historia ya kale tangu kuumbwa kwa ulimwengu, historia ya Dola ya Uajemi mpaka kuingia kwa utawala wa Kiislamu katika karne ya saba.

 Alipokuwa na umri wa miaka 23 tu, alipata “Shahnameh” iliyoandikwa na Abu-Mansour Almoammari; ambayo haikuwa katika umbo la kishairi. Ilijumuisha matoleo ya zamani yaliyoamriwa na Abu-Mansour ibn Abdol-razzagh. Ferdowsi alianza utunzi wake wa Shahnameh katika enzi ya Samanid mnamo 977 Miladia.

Baada ya miaka 30 ya kazi ngumu, alimaliza kuandika kitabu hicho na miaka miwili au mitatu baada ya hapo, Ferdowsi alikwenda Ghazni, mji mkuu wa Ghaznavid, kuwasilisha kitabu hicho kwa mfalme. Kwa mujibu wa wanahistoria, Mfalme alimuahidi Ferdowsi dinari kwa kila disti iliyoandikwa katika Shahnameh, kwa jumla ilibidi alipwe (dinari elfu sitini), lakini baadaye mfalme alighairi na kumkabidhi (dirham elfu ishirini ), ambazo wakati huo zilikuwa na thamani ndogo sana kuliko dinari. Kwani kila dirham mia moja zilikuwa na thamani ya dinari moja. Alikuwa amemuachia Mfalme Mahmoud wa Ghazni, shairi refu aliloliandika kwa hisia kali na kulibandika kwenye ukuta wa chumba alichokuwa akifanya kazi ya uandishi wa shahnameh yake kwamba, nanukuu; "Kisasi cha mbinguni hakitasahau. Punguza jeuri kutoka kwa maneno yangu ya moto, na utetemeke kwa hasira ya mshairi." Mwisho wa kunukuu.

Licha ya kuungwa mkono na wale waliopendezwa na historia na fasihi ya kale huko Khorasan, Ferdowsi alidharauliwa sana na kutupwa mkono katika miaka ya mwisho ya maisha yake. Sababu moja ni kutokuwa na fadhila Sultan Mahmud wa Ghazni, na sababu nyingine ilikuwa masuala ya kiitikadi, kwani Abolqasem Ferdowsi alikuwa Muislamu wa Madhehebu ya Shia.

 

Ferdowsi inasemekana alikufa takribani mwaka 1020 Miladia katika hali ya ufukara na umaskini mkubwa akiwa na umri wa miaka 90. Mazishi ya Ferdowsi katika Makaburi ya Tous yalizuiwa; kwa sababu wakati huo mazishi ya Waislamu wa Madhehebu ya Shia katika makaburi hayo yalipigwa marufuku. Hatimaye, Ferdowsi alizikwa katika ua wa nyumba yake na baada ya muda, kaburi lake liliharibiwa,na ilipofika mwaka 1307 hadi 1313 Miladia, kwa amri ya Reza Shah Pahlavi na Jumuiya ya Turathi ya Utamaduni, kaburi la Ferdowsi lilijengwa upya.

Maelezo ya mwisho ya maisha ya mshairi huyo yanasikitisha kwani Ferdowsi alikufa akihisi kuwa alikuwa ametumiwa vibaya na wale aliokuwa akiwategemea sana. Alikuwa katika hali mbaya kiafya kwa muda mrefu kabla ya kupatwa na mshtuko wa moyo, na kufariki dunia.

Baada ya Ferdowsi kufariki dunia, mfalme kwa aibu alituma tena pesa katika kijiji cha Ferdowsi, lakini wajumbe walipofika nyumbani kwake, walimkuta tayari ameshafariki dunia. 

Ferdowsi ana nafasi ya pekee katika historia ya Uajemi kwa sababu ya hatua alizopiga katika kufufua lugha ya Kiajemi na mila za kitamaduni, na kazi zake zimetajwa kama sehemu muhimu katika kuendelea na kuenea kwa lugha ya Kiajemi. Katika suala hili, Ferdowsi anawapita kwa mbali malenga wengine wa Kiirani kama vile Nezami, Khayyam, Asadi Tousi, na wanafasihi wengine wa fasihi wa Kiajemi katika athari zake kwa utamaduni na lugha ya Kiajemi. Wairani wengi wa zama zetu hizi wanamuona Ferdowsi  kama baba wa lugha ya kisasa ya Kiajemi, na kama malenga na mshairi mkuu zaidi wa washairi. Muhimu zaidi kuliko yote, kitabu chake cha Shahnameh kimesalia katika nyumba na mioyo mingi ya Wairani.

 

Kwenye moja ya beti zake ameeleza kuwa, “... Niliteseka katika miaka hii thelathini, lakini nimewafufua Wairani (Waajemi) kwa lugha ya Kiajemi; Sitakufa kwa vile niko hai tena, kwani nimeeneza mbegu za lugha hii ... "

Abolqasem Ferdowsi alipomaliza kuandika Shahnameh yake aliandika maneno haya kama hitimisho la utenzi wake huo, na hapa tunanukuu:

"Nimefika mwisho wa historia hii kuu,

Na nchi yote itajaa mazungumzo juu yangu,

Sitakufa, bali mbegu hizi nilizopanda zitaokoa

Jina langu na sifa zangu nikiwa kaburini,

Na watu wenye akili na hekima watatangaza

 sifa zangu na umaarufu wangu nitakapoondoka duniani".

 

Kaburi la Ferdowsi liko umbali wa kilomita 20 kaskazini-magharibi mwa Mashhad, njiani kuelekea Kalat Naderi, karibu na mji wa kihistoria wa Tabaran.

Kila mwaka, inapofika tarehe 25 Ordibehesht kwa kalenda ya Kiirani, sawa na tarehe 15 Mei, huwa ni siku ya kumuenzi mtaalamu huyu wa fasihi na malenga mkubwa wa Kiirani.

JIna Hakim Abulqasim Mansour Ferdowsi
Nchi Iran
FERDOWSI MALENGA NA MSHAIRI WA KIIRANI
319 Hijiria Shamsia
kaziHakim Abulqasim Mansour Ferdowsi mtaalamu wa fasihi na malenga mkubwa wa Iran, alizaliwa mwaka 319

Jumuiya ya Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu ni moja ya mashirika ya Iran ambayo yanafungamana na Wizara ya Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu; na ilianzishwa mwaka 1995. [Ziada]

:

:

:

: