• Mar 22 2022 - 12:39
  • 227
  • Muda wa kusoma : 3 minute(s)
Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu na kauli mbiu ya mwaka mpya

Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu na kauli mbiu ya mwaka mpya

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyid Ali Khamenei, ametoa ujumbe kwa mnasaba wa kuanza mwaka mpya wa 1401 Hijria Shamsia na akaupa mwaka huo jina la mwaka wa "Uzalishaji wa Kutegemea Teknolojia na Utengenezaji Ajira".

Ayatullah Khamenei ametaja kuwa ni moja ya mafanikio ya mwaka 1400 hatua kubwa iliyochukuliwa kukabiliana na janga la corona na akaelezea mafanikio mengine makubwa katika mwaka huo kwa kusema: katika sekta mbalimbali za sayansi na teknolojia zilifanyika kazi kubwa kuanzia utengenezaji wa aina kadhaa za chanjo za kuaminika mpaka urushaji wa satalaiti.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameema, lengo la kuainisha kaulimbiu maalumu ya mwaka ni kuwafanya viongozi, vyombo husika na wananchi wote wawe na muelekeo katika ufanyaji mambo na akaitaja sababu ya kujikita zaidi kwenye suala la uzalishaji katika miaka ya karibuni kwa kusema: uzalishaji ni ufunguo wa kutatulia matatizo ya kiuchumi na njia kuu ya kuvukia misukosuko ya kiuchumi. Lakini pia ukuaji wa uchumi, uongezaji ajira, upunguzaji mfumuko wa bei na ughali wa maisha, uongezaji pato la mtu mmoja mmoja, kuboresha ustawi wa jamii na vilevile kuongeza moyo wa kujiamini na heshima ya kitaifa, yote hayo yanafungamana na ustawi mkubwa na mpana wa kile kinachoitwa Uzalishaji wa Kitaifa, ambao kuutegemea kwake katika miaka hii kumekuwa na taathira nzuri.

 

Ayatullah Khamenei ameongezea kwa kusema: "mwaka huu pia ninaendelea kutilika mkazo suala la uzalishaji. Tab'an kwa kutumia njia mpya ya uzalishaji, yaani uzalishaji wa "kiteknolojia" na "utengenezaji ajira".

Amefafanua kwamba, kulitumia kama kipimo suala la uzalishaji wa kutegemea teknolojia na wa kutengeneza ajira kunawezesha kupiga hatua mbele na kwa namna inayoweza kuhisika katika kufikia malengo yote ya kiuchumi; na akaongezea kwa kusema: kaulimbiu ya mwaka 1401 ni: "uzalishaji; utegemeaji teknolojia, utengenezaji ajira".

Sisitizo la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu juu ya suala la uzalishaji wa kitaifa kuwa ufunguo wa kuondokana na matatizo ya kiuchumi kama mfumuko wa bei na ughali wa maisha na kuweza pia kufikia malengo muhimu kama kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na kuboresha hali ya ustawi wa jamii, kunapata maana yake halisi tunapozingatia uwezo mbalimbali ilionao Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyuga na nyanja tofauti za uzalishaji kama rasilimaliwatu bingwa na mahiri, utajiri mkubwa wa maliasili za nishati kama mafuta na gesi pamoja na bidhaa zitokanazo na nishati hizo, kuwepo miundomsingi mikubwa na ya aina mbalimbali nchini, utaalamu wa kiufundi na kiujuzi; na muhimu zaidi kuliko yote hayo, kuwepo kwa moyo na azma ya kitaifa katika nchi nzima ya kutaka kufikia kiwango cha kujitosheleza na kujitegemea na kukata utegemezi kwa wageni hususan katika mahitaji ya kistratejia.

Katika sekta ya kilimo pia, Iran inao uwezo mkubwa kutokana na kubarikiwa ardhi kubwa na yenye rutuba, anuai za hali ya hewa na nguvukazi nyingi; na endapo itatekelezwa mikakati mikubwa na iliyoratibiwa katika utumiaji maji na mipango makini katika matumizi ya ardhi za kilimo si tu itawezekana kukidhi mahitaji ya nchi kwa bidhaa za kistratejia kama ngano, shairi, mahindi, mafuta ya kupikia na pembejeo za mifugo, lakini pia itawezekana kusafirisha na kuuza bidhaa hizo nje ya nchi.

Suala jengine ambalo Ayatullah Khamenei amelitilia mkazo ni kwamba, uzalishaji wa kitaifa inapasa usimame juu ya misingi miwili ya kutumia teknolojia na kubuni nafasi za kazi. Katika zama hizi, ambapo ujuzi na utaalamu wa mwanadamu unaongezeka kiwango na ubora kwa kasi ya kustaajabisha, kulipa umuhimu suala la elimu na teknolojia katika uga wa uzalishaji katika nyanja zote, kuanzia kilimo hadi sekta za viwanda, nishati na nyenginezo, maana yake ni kutilia mkazo utumiaji wa mafanikio ya karibuni kabisa ya elimu yaliyopatikana hasa katika teknolojia za kisasa kama nano, teknolojia za kompyuta, selishina, metolojia, makrobiolojia, kwantam, teknolojia za matumizi ya amani ya nyuklia, seli za jenetiki na elimu ya jenetiki; taaluma ambazo vijana bingwa na wataalamu wa Kiirani wameshaweza kuzifikia; na hivyo kuzitumia zote hizo kwa wingi na kwa ubora zaidi katika uzalishaji wa kitaifa.

Si hayo tu, lakini kwa kutilia maanani pia kwamba ukosefu wa ajira ni miongoni mwa matatizo sugu, kuufanya uzalishaji wa kitaifa kuwa dira kuu ya hatua zinazochukuliwa na Serikali na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na wananchi wenyewe wa Iran, kunaweza kuwa na taathira kubwa katika kulipatia suluhisho la msingi tatizo hilo. Kwa kuwapatia ajira wananchi wa matabaka mbalimbali katika sekta tofauti za uzalishajil kutaandaa mazingira ya kutatua masuala mengine ya kijamii likiwemo la kuoa kwa vijana.../

تانزانیا دارالسلام

تانزانیا دارالسلام

Andika maoni yako.

Ingiza maandiko yako Kisha bonyeza Enter

Mabadiliko ya ukubwa wa maandiko:

badilisha nafasi za maneno:

Badilisha urefu wa mistari:

Badilisha aina ya panya: