• Aug 2 2023 - 15:42
  • 352
  • Muda wa kusoma : 10 minute(s)
Maulidi S. Sengi

Siku ya Ashuraa

Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi la batili ili kuilinda dini ya Allah. Hamasa ya Karbala ilikuwa dhihirisho la mambo mawili makuu. Kwanza ni ujasiri, ushujaa, moyo wa kujitolea, uaminifu pamoja na kuyapokea kwa moyo mkunjufu mauti ya kuuawa shahidi, sifa walizojipamba nazo wapiganaji wachache wa jeshi la haki wakiongozwa na Imam Hussein AS dhidi ya Yazid bin Muawiya. Pili ni upeo wa ukatili, udhalimu na unyama ulioonyeshwa na jeshi batili la Yazid bin Muawiya. Baada ya kupambana kishujaa, hatimaye mjukuu huyo wa Mtume Muhammad SAW aliuawa shahidi katika siku kama ya leo.

Katika makala hii tutaangazia sehemu moja ya Falsafa ya Siku ya Ashura na harakati ya Imam Hussein AS

Falsafa ya Ashura

Je, ni nini  falsafa na malengo ya harakati na mapambano ya mtukufu huyo katika Siku ya Ashura katika ardhi ya Karbala?

Katika historia ya mwanadamu kuna vita vingi mno vilivyotokea. Kati ya hivyo, idadi ya mapambano yaliyoendeshwa kwa lengo la kutetea haki na uadilifu si haba wala si machache hata kidogo. Kuna watu wengi wapigania haki waliotoa mhanga roho zao na za wapendwa wao kwa ajili ya kusimamisha uadilifu na hata kwa ajili ya malengo ya kidini. Na ni hakika isiyo na shaka kwamba kila anayesimama imara kupambana katika njia ya haki ana malipo na ujira mbele ya Mola wa ulimwengu. Lakini baadhi ya watu hao hata majina yao hayajabakia katika historia; na baadhi ya wengine zimesalia kumbukumbu zao tu za kukumbukwa kwa wema katikka fikra za wanadamu. Kati ya mapambano yote ya kupigania haki yaliyoendeshwa na waja safi na wema, ni mapambano ya Imam Hussein AS tu ndiyo ambayo licha kupita miaka 1,400 kungali kuna mamilioni kwa mamilioni ya watu wenye mapenzi makubwa juu yake, ambao kila mwaka wanaomwomboleza na kumkumbuka kwa huzuni na majonzi makubwa. Mapambano ambayo sha'ar na thamani zake daima zimebaki kuwa chemchemi na chachu ya mabadiliko na mageuzi makubwa mno duniani. Viongozi wakubwa wa dini wanaitakidi kuwa siri ya kuendelea kubakia kumbukumbu hiyo ni ikhlasi aliyokuwa nayo Imam Hussein AS pamoja na wafuasi wake. Kwa sababu amali pekee zenye thamani mbele ya Mwenyezi Mungu ni zile zinazofanywa kwa ajili ya kupata radhi za Mola.

Qur’ani Tukufu

Ndani ya Qur'ani tukufu maamrisho yote ya kidini yamefungamanishwa utekelezaji wake na ikhlasi na kujikurubisha kwa Allah SWT. Kama ambavyo Mola Mwenyezi anaizungumzia Jihadi ndani ya Kitabu chake hicho kitukufu kwa kusema :"Wale waliopigana Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu"; aidha kuhusu kufa shahidi akasema: "Wale waliouawa katika njia ya Mwenyezi Mungu"; na katika utoaji mali pia akasema: "Wale wanaotoa mali zao katika njia ya Mwenyezi Mungu". Lakini pia kama tunavyosoma ndani ya Qur'ani tukufu katika aya ya 9 ya Suratu Dahr kuhusu Ahlul Bayt wa Bwana Mtume Muhammad SAW pale walipoamua kutoa chakula chao pamoja na kukipenda mno na kukihitajia, wakampa masikini, yatima na mateka aliyeachiwa huru na wakasema ndani ya nafsi zao: "Hakika sisi tunakulisheni kwa ajili ya kutaka radhi za Mwenyezi Mungu tu. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani."

Na hii ndiyo iliyokuwa sifa kuu iliyopamba harakati ya Imam Hussein AS pia, kwamba ilitekelezwa kilillahi na kwa ikhlasi kwa ajili ya Allah na dini yake bila ya kuchanganyika na hata chembe ya lengo jingine lolote lile. Qur'ani tukufu inasema katika aya ya 47 ya Suratul Anfal: "Wala msiwe kama wale walio toka majumbani mwao kwa fakhari na kujionyesha kwa watu". Na yeye mwenyewe Imam Hussein AS akaeleza haya kuhusiana na harakati yake: "Sikutoka mimi kwa ajili ya kutaka uongozi wala kufanya ufisadi, wala kufanya dhulma, bali nimetoka kupambana ili kurekebisha hali ya ummah wa babu yangu tu."

Wafuasi wa Imam Hussein AS

Katika mapambano na harakati hiyo ya kiikhlasi, wafuasi wenye ikhlasi pia ndio waliomsaidia Imam; amma wale ambao mbali na radhi za Mwenyezi Mungu walikuwa na mambo mengine pia waliyokuwa wakiyapigania, na nafsi zao zikawa zimeficha hata chembe ndogo tu ya utovu wa ikhlasi, hao, ima hawakujiunga kabisa na msafara huo au walimwacha mkono Imam Hussein katikati ya njia. Imam Hussein AS pamoja na wafuasi wake hawakuwa wakitafuta kitu kingine ghairi ya radhi za Mola wao Muumba; na hii ndio siri ya kuendelea kubaki kumbukumbu ya Ashura. Harakati na hamasa ya Ashura sio tu haijachakaa na kusahaulika kwa sababu ya kupita muda, bali mvuto na mng'aro wake unazidi kuongezeka siku baada ya siku; na hii ni kutokana na baraka za ikhlasi; kwa sababu katika mfumo wa uumbaji amali yenye ikhlasi haifutiki wala haitoweki.

Kwa nini Imam  Hussein AS alijitosa vitani?

Kwa kawaida kila mtu anayejitosa kwenye medani ya mapambano na kujipanga kukabiliana na adui hutaka apate ushindi na kumshinda adui yake. Katika hili, Imam Hussein (as) na wafuasi wake hawakuwa tofauti na watu wengine, bali nao pia walitaka watoke na ushindi katika medani ya Jihadi. Lakini kutokana na mazingira ya mahala na zama aliyokabiliana nayo, Imam Hussein (as) angeweza kweli kutoka na ushindi katika medani hiyo ya mapambano? Na kama hangeweza, kwa nini basi alijitosa katika medani hiyo? Katika kulijibu suali hili tunaweza kusema kwamba, ushindi katika Uislamu ni kufanikiwa kutekeleza wajibu wa kidini na kukamilisha mtu mas-ulia na dhima aliyonayo kisharia. Baadhi ya wakati, kutokana na hali inavyokuwa, mtu huwa hana budi kufanya lolote lile ili aweze kufikia lengo na makusudio yake hata kama hatima ya atakalofanya itakuwa ni mauti na kifo chake. Wapiganaji wa jeshi la Uislamu katika zama za mwanzoni mwa kudhihiri dini hiyo tukufu nao pia walikuwa wakishindana kwa kila mmoja kutaka kuwa wa mbele katika medani za Badr, Khaibar, Ahzab n.k kwa ajili ya kutekeleza amri ya Allah na kuuhami Uislamu; na wakijua kwamba hatima ya kujitolea na kushindana kwao huko kuwa wa mbele katika medani ya Jihadi ni kuuawa shahidi. Lakini kwa vile wakitambua kwamba hakuna njia nyingne kwa ajili ya kuihifadhi na kuilinda dini ghairi ya hiyo walijitosa kwenye medani hiyo isiyo na marejeo.

Imeelezwa katika hadithi nyingi kuwa endapo maisha ya Muislamu yatakuwa hatarini, basi aifanye mali yake ngao ya kuokolea maisha yake. Lakini kama dini ya Uislamu itakabiliwa na hatari muumini anatakiwa aifanye roho yake ngao ya kulindia dini yake. Kwa hivyo inajuzu kujitolea na kuitoa mhanga mtu nafsi yake kwa namna yoyote ile ili kuilinda dini yake; na hivyo ndivyo alivyofanya Imam Hussein AS.

Japokuwa Imam alikuwa na uelewa kamili wa hatima na mwisho wake na Ahlul Bayt zake katika njia ya kuelekea Karbala, lakini alikuwa akitambua kwamba kuilinda dini ni muhimu zaidi kuliko kunusuru roho yake. Upotofu ndani ya utawala ulioonekana kidhahiri kuwa wa Kiislamu wa Muawiya na baada yake mwanawe Yazid ulikuwa umefikia kiwango ambacho laiti kama Imam Hussein AS na wafuasi wake waaminifu wasingesimama kupambana, Uislamu, Qur'ani na kila kilicholetwa na Mitume katika zama mbalimbali za historia kingezikwa chini ya kifusi cha bid'a, uzushi na upotofu ulioletwa na watu hao; na wala isingebakia athari yoyote ya mafunzo hayo asili. Kama ambavyo dini zilizopita pia zilizikwa chini ya vihame na magofu ya historia pasina kubakia athari yoyote ya mafundisho yao sahihi. Kwa sababu hiyo Imam Hussein (as) aliyatoa mhanga maisha yake, ya watu wa nyumba yake na masahaba zake ili dini ya Mwenyezi Mungu iendelee kubaki hai na ili misingi na asili yake iendelee kuwepo. Na ni namna hivi mapambano na hamasa hiyo imebakia milele katika kurasa za historia na kuwa kigezo cha kufuatwa na mujahidina wote wa njia ya haki na uadilifu.

Barua kwa Habib ibn Madhahir

Wakati Imam Hussein (as) alipowasili Karbala alimwandikia barua Habib Ibn Madhahir ambaye alikuwa sahaba wa Bwana Mtume SAW na sahiba wa karibu wa baba yake, yaani Imam Ali bin Abi Talib AS; na ndani ya barua hiyo akamwambia: "Ewe Habib! wewe ni muelewa zaidi wa ukuruba wangu na Mtume wa Allah na unatujua sisi zaidi kuliko watu wengine. Kwa upande mwingine, wewe u mwelewa wa yaliyotusibu na ni mtu mwenye ghera. Kwa hivyo usiache kutoa msaada wako kwetu. Babu yangu Mtume wa Allah atakuenzi Siku ya Kiyama."

Wakati barua ya Imam ilipomfikia Habib, kwa kuhofia shari ya askari wa Ubaidullah Ibn Ziyad, sahaba huyo wa Bwana Mtume alijifanya mgonjwa na kujionesha mbele ya watu wa kabila wake kuwa kwa uzee alionao hawezi tena kufanya chochote. Habib Ibn Madhahir alikuwa akizungumza namna hiyo ili uamuzi aliokuwa nao moyoni mwake usije ukajulikana na ili aweze kunusurika na shari ya Ubaidullah. Hatimaye Habib aliondoka mji wa Kufa kimyakimya wakati wa usiku na kuelekea Karbala pamoja na mtumwa wake.

Wakati Habib Ibn Madhahir alipofika Karbala alionyesha katika medani ya matendo utiifu na uaminifu wake kwa Imam Hussein AS. Mara tu alipobaini kuwa idadi ya wafuasi wa Imam Hussein ni wachache na maadui ni wengi mno alimwambia Imam: "Karibu na hapa kuna watu wa kabila la Bani Asad. Kama utanipa idhini nitawaendea kuwatolea wito wa kukusaidia. Huenda asaa Mwenyezi Mungu akawafanya wauone uongofu". Baada ya Imam Hussein kutoa idhini, Habib alielekea haraka haraka kwa watu hao kuwapa nasaha na mwongozo kwa kuwaambia: "Nimekuleteeni hidaya njema; ni kitu bora kabisa ambacho kiongozi wa kaumu anawapelekea watu wake. Ni huyu Hussein, mwana wa Amirul Muuminin na Fatimatu-Zahraa, ambaye amefikia kando na karibu yenu; wameandamana pamoja naye idadi ya waumini huku maadui zake wakiwa wamemzingira kwa nia ya kutaka kumuua. Nimekuja kukuiteni mukamhami na kulinda heshima ya Mtume kuhusu yeye. Wallahi! kama mtamsaidia, Mwenyezi Mungu atakupeni utukufu duniani na akhera". 

Mmoja wa watu hao aliyekuwa akiitwa Abdullah Ibn Bashir alisimama na kusema: "Ewe Habib, Mwenyezi Mungu akulipe kwa juhudi zako! Umetuletea fahari kubwa ambayo mtu huwaletea watu wake walio azizi zaidi kwake!  Mimi ni mtu wa mwanzo kabisa ninayeuitikia wito wako.... " Kwa namna hiyo watu wengine, nao pia walisimama wakasema kama aliyoyasema yeye na kutangaza kuwa wako tayari kuungana na kumsaidia Imam Hussein (as), ambapo idadi ya watu hao inasemekana ilifika 70 au 90. Walichukua uamuzi wa kuelekea Karbala, lakini majasusi wasaliti miongoni mwao walikwenda kumpa ripoti Omar Saad, ambaye alimteua mtu katili na asiye na huruma aitwaye Azraq afuatane na askari wapanda farasi 500 ambao usiku wa siku ileile walifika kwa watu wa kabila la Bani Asad na kuwazuia wasiweze kuondoka. Japokuwa watu hao hawakuweza kwenda kumpa msaada Imam Hussein, lakini baada ya tukio la Ashura na kufanywa mateka watu wa Nyumba ya Bwana Mtume SAW, walielekea ardhi iliyotapakaa damu ya Karbala na kuvizika viwiliwili vitoharifu vya mashahidi.

Malipo kutoka kwa Mwenyezi Mungu

Amma Habib Ibn Madhahir, mja mwenye ikhlasi na imani ya kweli alisimama kupambana na adui; alipiga ukelele mkali wa hamasa na kuingia kwenye medani ya mapambano. Yalikuwa mapigano makali kati ya Habib na jeshi la watu wenye chuki na uadui, ambapo ghafla mtu mmoja wa kabila la Bani Tamim alimshambulia Habib na kumpiga upanga wa kichwa. Wakati huohuo mtu mwingine wa jeshi la adui alimpiga mkuki mtukufu huyo akaanguka chini. Habib alitaka kuinuka, mara Haswin bin Tamim akamkata kichwa chake na kukitenganisha na kiwiliwili chake na Habib akafikia daraja tukufu ya kufa shahidi. Kufa shahidi kwa mzee huyo mwenye mapenzi makubwa ya Mola wake ulikuwa msiba mkubwa mno kwa wafuasi wa Imam Hussein AS na yeye Imam mwenyewe. Wakati Imam Hussein alipokifikia kiwiliwili kitoharifu kisicho na kichwa cha Habib Ibn Madhahir alisema: "Malipo yangu na wafuasi wangu wanaonisaidia nataraji kuyapata kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu"

تانزانیا دارالسلام

تانزانیا دارالسلام

Andika maoni yako.

Ingiza maandiko yako Kisha bonyeza Enter

Mabadiliko ya ukubwa wa maandiko:

badilisha nafasi za maneno:

Badilisha urefu wa mistari:

Badilisha aina ya panya: