Maulidi Sengi
Rais Samia akutana na Waziri wa Mambo ya nje wa Iran
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mhe. Amir Abdlollahian Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 26 Agosti, 2022.
Katika kikao hicho cha Ijumaa, Rais wa Tanzania na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran wamefanya mazungumzo kuhusu uhusiano wa nchi mbili na pia kuhusu masuala ya kimataifa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kustawisha uhusiano wa pande zote na nchi za Afrika hasa Tanzania ni kipaumbele katika sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Huku akiashiria uwezo mkubwa wa Iran kiuchumi hasa katika nyuga za biashara, nishati, viwanda, teknolojia na vyuo vikuu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametoa wito wa kuondolewa vikwazo kwa mashirika na wafanyabiashara wa Iran nchini Tanzania hasa katika masuala ya visa.
Kwa upande wake, Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na ujumbe aliokua ameandamana nao ambapo ametaka kuimarishwe mabadilishano ya kibiashara na kiuchumi baina ya Iran na Tanzania. Aidha amekubali mwaliko rasmi wa kuitembelea Iran kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa kuna mpango wa kufanya safari hiyo kabla ya kumalizika mwaka huu wa 2022.
Mapema Ijumaa pia Waziri wa Mambo ya Nje wa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Hussein Mwinyi wa Zanzibar na wawili hao wakasitizia udharura wa kuimarishwa ushirikiano baina ya pande mbili.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliwasili nchini Tanzania Jumatano usiku na kusema kwamba kunatayarishwa ramani ya njia kuhusiana na kuimarisha uhusiano wa Iran na Tanzania ili mchakato huo uchukue mkondo wa kasi.
Wakati huo huo baada ya safari hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Jumamosi kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa, uhusiano wa Tehran na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unazidi kuwa imara.
Andika maoni yako.