maulidi
Mazazi ya Imam Mahdi (AJTFS)
Imam Muhammad Mahdi (a.s) alizaliwa siku ya Ijumaa ya mwezi 15 Shaaban mwaka 255 Hijria mjini Samarra Iraq na baba yake akiwa ni Imam Hassan Askari (a.s). Imam Mahdi ni mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w) kupitia kizazi cha masharifu na masayyid cha binti mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad y
Imam Muhammad Mahdi (a.s) alizaliwa siku ya Ijumaa ya mwezi 15 Shaaban mwaka 255 Hijria mjini Samarra Iraq na baba yake akiwa ni Imam Hassan Askari (a.s). Imam Mahdi ni mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w) kupitia kizazi cha masharifu na masayyid cha binti mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad yaani Bibi Fatimatu Zahra (alayha salaam). Mama yake alikuwa Bibi mwenye heshima kubwa aliyejulikana kwa jina la Nargis. Imam Mahdi (a.s) ni nyota ya 12 ya Maimamu wa Ahlul Bayt (a.s) waliousiwa na Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Ilikuwa ni katikati ya mwezi wa Shaaban, pole pole mbingu zilikuwa zinaanza kutoa fursa ya kupuliza upepo mwanana wa alfajiri. Ilikuwa muonzi wa dhahabu wa kuchomoza jua bado haujapasua kifua cha upeo wa macho; alipozaliwa mtukufu huyo. Bila ya kukusudia, udongo wa ardhi ulianza kunukia harufu ya umaanawi. Mzizimo ulienea kila mahala. Kitoto kichanga kikaanza kuonyesha makarama yake kwa kunyoosha kidole chake cha shahada mbinguni na kusema, Alhamdulillahi Rabbil Alamin, Waswalallahu Alaa Muhammadin Waalih.
Tunapozingatia historia ya mwanadamu tunatambua kwamba kufr, ujahili, dhulma, ghasia na umasikini ndizo changamoto kuu ambazo zimekuwa zikiikumba jamii ya mwanadamu. Katika upande wa pili, msingi wa serikali ya Imam Mahdi (a.s) utalenga kuvunja na kuondoa kabisa changamoto hizo. Kwa ibara iliyo wazi zaidi ni kuwa mtukufu huyo atakuja kwa lengo la kueneza fikra ya tauhidi, kueneza elimu, kuvunja misingi ya dhulma, kuwaonyesha wanadamu utamu wa uadilifu, kuwaonyesha njia ya salama na hatimaye kuwafikisha kwenye maisha bora yaliyojaa saada ya milele.
“Ewe Mwenyezi Mungu mmiminie rehema zako Walii Wako, uliyempa majukuu ya kusimamia masuala ya waja Wako, Imam anayesubiriwa, Imam Mahdi (a.s). Ewe Mola wetu msheheneze baraka Zako na utufanye azizi kwa kudhihiri kwake, umsaidie; na kupitia kwake utusaidie na sisi, umpe nusura Yako kamili na nguvu za kuweza kuikomboa kirahisi dunia, na umpe kutoka Kwako cheo na nguvu. Ewe Mola wetu itie nguvu dini Yako na sunna za Mtume Wako kupitia kwake, ili kisibakie chochote katika dunia ghairi ya haki. Ewe Mwenyezi Mungu wape nguvu Waislamu na wapenda haki na uwadhilishe madhalimu na watu wa batili na utuingize peponi kwa rehema Zako”.
Andika maoni yako.